Kikosi cha wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika timu ya soka Yanga.
Wadau wa michezo hapa nchini wameziangalia timu za Yanga SC ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika na Azam FC wanaoiwakilisha nchini katika michuano ya kombe la shirikisho nakusema timu hizo zinakibarua kizito katika michezo yao ijayo ya hatua ya 16 bora.
Wakizungumzia michezo hiyo ambayo itapigwa nchini kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao baadhi ya wadau hao wamesema timu za waarabu hasa kongwe kama El Ahly ya Misri itakayovaana na Yanga na Esperance ya Tunisia itakayovaana na Azam ni timu ambazo zinauzoefu wa muda mrefu na michuano ya vilabu barani Afrika CAF na wanakuwa na mipango mingi ya ndani na nje ya uwanja na isiyo ya kimpira ili mradi kuhakikisha wanapata matokeo yakusonga mbele.
Yanga itamenyana na wababe wao wa kihistoria katika michuano ya Afrika, Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Aprili 9, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana Aprili 19, Cairo, Misri.
Na baada ya Ahly kuinyanyasa kwa miaka mingi Yanga kwenye michuano yote ya CAF, safari hii wana Jangwani wamepania kuvunja mwiko kwa kuhakikisha wanawang’oa Waarabu hao.
Ahly imefuzu hatua hii baada ya kuitoa Recreativo do Libolo ya Angola kwa ushindi wa jumla wa 2-1, iliyoupata Cairo baada ya sare 0-0 Angola, wakati Yanga imeitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 2-1 Kigali na kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2014 katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa penalti 4-3, baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
Kwa upande wa Azam fc wao watavaana kwa mara ya kwanza na timu ya Esperance ya Tunisia yenye uzoefu mkubwa na ngarambe za michuano hiyo huku timu zote zikitakiwa kujifunga kibwebwe na kuweka mikakati mizito na thabiti yakuziwezesha kuibuka na ushindi mnono wa nyumbani na hivyo kujirahisishia kazi katika michezo ya marudiano ugenini.
Ikumbukwe katika historia ya soka barani Afrika klabu ya soka ya Simba ndiyo timu pekee Tanzania yenye rekodi ya kuweza kuwaondosha waarabu katika michuano ya CAF, ikiwahi kufanya hivyo katika michuano ya shirikisho zamani kombe la CAF mnamo msimu wa mwaka 1993-94 ilipowaondosha Arab Contractors ya Misri katika hatua ya awali na Simba kufika fainali na kupoteza mbele ya Stellah Abjan ya Ivory Coast.
Siamba kwa mara nyingine mnamo mwaka 2003 iliweza kukiangusha kigogo kingine cha Misri timu ya Zamaleki na kusababisha mstuko mkubwa katika soka barani Afrika baada ya kuitupa timu hiyo katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika.
Na mara nyingine timu ya Simba mnamo mwaka 2012 ilifanikiwa kuwatoa kimasomaso Watanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika CAF baada ya kuitupa nje timu ngumu kabisa ya Es Setif ya Algeria japo haikiuwa kazi rahisi.
Hivyo wadau kwa kuzingatia uzefu na ubora wa wapinzani hao wamezitaka timu hizo kufanya maandalizi ya ukweli na mipango mikakati ya ushindi sio kufanya maandalizi ya mbwembwe na baadae kujikuta zikifungashwa virago mapema.
Wakimalizia wadau hao wamesema kimsingi katika soka lolote laweza kutokea ndani ya dakika tisini za mchezo mahali popote iwe nyumbani ama ugenini na hata hao waarabu wanajua wanakazi ya kufanya mbele ya Watanzania na ndio maana wamekuwa na tabia yakutuma mashushushu kuja kutazama michezo ya timu zetu.