
Ruvu Shooting na Yanga, katika dimba la taifa leo
Mabao ya Yanga yamefungwa na Saimon Msuva dakika ya 31 kwa mkwaju wa penati uliopatikana baada ya beki wa Ruvu kuunawa mpira katika eneo la hatari, huku la pili likifungwa kwa ustadi mkubwa na Emmanuel Martin dakika ya 90+4 kwa kichwa akimalizia kros ya Saimon Msuva.
Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 52 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukamata nafasi ya pili, nyuma ya vinara Simba SC wenye pointi mbili zaidi ingawa nao wamecheza mara 23.
Yanga iliyopoteza mechi ya tatu pekee msimu huu leo wangeweza kuvuna mabao zaidi kama si maamuzi ya utata ya waamuzi pamoja na umakini wa washambuliaji wake ambapo ilimaliza dakika 45 ikiwa pungufu, baada ya mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa kuoneshwa kadi mbili za njano za utata ndani ya dakika mbili na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 45.
Obrey Chirwa
Chirwa alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 44 baada ya kuifungia Yanga bao lingekuwa la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Hassan Kessy, lakini mwamuzi Ahmada Simba kutoka Kagera akalikataa na kumuonesha kadi ya njano, kwa madai kuwa Chirwa alifunga bao hilo kwa mkono.
Dakika mbili baadaye Mzambia huyo akaonyeshwa kadi ya pili njano dakika ya 45+1 baada ya kuudunda mpira chini kwa hasira na hatimaye kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe pia akaifungia Yanga bao dakika ya 47 lakini lakini alikuwa ameotea, na mwamuzi kulikataa bao hilo.