Jumatano , 30th Jan , 2019

Klabu ya Yanga imeeleza kuwa inashangazwa na kitendo cha Kakolanya kutoonekana klabuni hapo wakati alilipwa stahiki zake lakini yeye akasisitiza kuwa anataka kuvunja mkataba ili awe huru.

Kakolanya

Hilo imethibitishwa na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga Samuel Lukumay, ambaye amesema ni kweli Beno kupitia kwa mwanasheria wake aliiandikia Yanga ya kutaka kuvunja mkataba.

''Beno ni mchezaji wetu ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili kuanzia msimu huu lakini alikaa kimya na mwisho wa siku akaandika barua ya kutoa notisi ya siku 14 ili kulipwa stahiki zake na tulimlipa bahati mbaya akaendelea kukaa kimya'', amesema.

Aidha Lukumay amesisitiza kuwa walishangaa baada ya kumlipa stahiki zake za miezi aliyokuwa anadai hakurejea kazini na mwanasheria wake akatuandikia barua akisisitiza kuwa mteja wake anataka kuvunja mkataba.

Kakolanya hajaitumikia Yanga tangu mwezi Novemba mwaka 2018 alipojiunga na kambi ya timu ya taifa kwaajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Lesotho ambapo hakurejea klabuni baada ya mchezo kupita.

Hata hivyo kocha wa Yanga Mwinyi Zahera aliwahi kuweka wazi kuwa hamhitaji mlinda mlango huyo hivyo atafute timu ya kujiunga nayo.