Ijumaa , 9th Nov , 2018

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) na klabu ya Yanga wamefikia makubaliano juu ya uchaguzi wa klabu hiyo ambao umepangwa kufanyika Januari 13, 2019.

Viongozi mbalimbali wa TFF kwenye mkutano na wanahabari.

Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na TFF leo, Novemba 9, 2018 uchaguzi huo utafanyika bila ya kujali kupingwa na baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga. 

Yanga na TFF wamekubaliana kuwa Kamati zote mbili za uchaguzi yaani ile ya TFF na ile ya Yanga zitashirikiana kusimamia uchaguzi huo.

Kwa upande wa wanachama ambao wamekuwa wakisisitiza kumtambua mwenyekiti wa zamani Yusuf Manji, wameshauriwa wamshawishi au kumchukulia fomu ili aweze kugombea tena nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine pia kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga imemteua Thobias Lingalangala kuwa kaimu mwenyekiti wa klabu hiyo hadi uchaguzi wa kujaza nafasi utakapofanyika januar 13.

Lingalangala amesema uchaguzi utafanyika kama ulivyotangazwa na kamati ya uchaguzi ya TFF na fomu zimeanza kutolewa rasmi leo katika ofisi za TFF na makao makuu ya Yanga.

Gharama za fomu nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti ni laki 2 huku gharama za wagombea wa nafasi ya ujumbe ni laki 1.

Uchaguzi huo utahusisha nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na nafasi nne za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kama taarifa ya Yanga inavyojieleza hapo chini.