Alhamisi , 30th Sep , 2021

Raundi ya kwanza ya Ligi Kuu soka Tanzania bara msimu wa 2021-22 ilikamilika kwa michezo miwili kuchezwa jana na kutimiza idadi ya michezo 8 iliyochezwa.

Wachezaji wa Yanga na Kagera wakiwania mpira

Ni timu mbili tu katika raundi ya kwanza zilizofanikiwa kufunga mabao mawili (2) huku timu 8 zikiwa hazijafunga na tayari yamefungwa mabao 10.

Timu hizo ni Polisi Tanzania na Namungo FC ndio zilizofanikiwa kufunga mabao 2 kwenye michezo yao, Namungo waliifunga Geita 2 - 0 na Polisi waliifunga KMC bao 2-0.

Yanga na Mbeya kwanza ndio timu pekee zilizoshinda ugenini, Mbeya kwanza waliifunga Mtibwa Sugar Bao 1-0 na Yanga walishinda ugenini dhidi ya Kagera Sugar kwa bao 1-0.

Raundi ya kwanza imeonekana kuwa ngumu hususa kwa vilabu kama Azam FC, Simba SC zote zimebanwa mbavu kwenye michezo yao ya ufunguzi kwa kupata sare, lakini pia timu kama KMC, Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting zote zimeanza kwa kufungwa.

Lakini pia tumeanza kushuhudia uhaba wa mabao mapema tu licha ya timu vigogo kusajili washambuliaji wa kigeni wanaotajwa kuwa bora katika eneo hilo,lakini katika michezo 8 iliyochezwa ya raundi ya kwanza yamefungwa mabao 10, ukiwa ni wastani wa bao 1.25 kwa mchezo..

Msimu mpya wa TPL ulianza kutimua vumbi Jumatatu Septemba 27 kwa michezo ya raundi ya kwanza, na msimu huu unatarajiwa kuwa ni msimu utakao kuwa na ushindani kutokana na maandalizi ya vilabu lakini pia uwepo wa uhakika wa kila klabu kupata pesa isiyopungua Milioni 500 kutoka kwenye pesa za matangazo ya haki za televisheni za TPL, kitu ambacho kitaviwezesha vilabu kuwa vizuri kiuchumi ikiwemo kulipa mishahara ya wachezaji.