Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo wamefanya mapokezi ya uongozi mpya wa chama hicho kupitia uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu kuanzia 21 Januari ambapo umeshuhudia ukomo wa madaraka ya Mwenyekiti wa muda mrefu wa chama hicho Freeman Aikeli Mbowe akishindwa uchaguzi huo dhidi ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake na mgombea Urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 Tundu Lissu.
Kati yaliyozungumzwa kwenye mapokezi hayo suala la umoja kwa Wanachadema halikuachwa nyuma ambapo Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu amewataka wanachama wa chama hicho kusahau mikwaruzano waliyopitia katika uchaguzi na kwenda mbele kukijenga chama.
Akizungumza baada ya kupokelewa Makao Mkuu ya chama hicho Mikocheni Dar Es Salaam Lissu amesema
“Sababu iliyofanya tusemezane vibaya imepita, sababu iliyotufanya tuvutane imepita na imepita kwa namna ambayo nchi hii nzima inaisifia. Nchi nzima hii inatusifia kwa hiyo kwa sababu tumefanya jambo ambalo kila mtu anatusifia bado tuna sababu ya kuvutana? hapana. Tunarudi wote nyumbani kwa sababu wote ni wa nyumba moja kwa hiyo baada ya kelele yote hii turudi nyumbani kwetu(CHADEMA) tuangalie palipobomoka tukajenge palipopasuka tuparekebishe wote."
Makamu Mwenyekiti mpya wa CHADEMA John Heche naye alikuwa na haya ya kusema kuwa chama hicho kitashirikiana na kila mwanachama na yeyote mwenye nia ya kufanya nacho kazi bila kuangalia aliwaunga mkono yeye au Mwenyekiti wa sasa Tundu Lissu katika kipindi uchaguzi.
Akizungumza leo Januari 29 2025 kwenye mapokezi ya Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu, Makao makuu ya CHADEMA Mikocheni Dar Es Salaam, Heche amesema
"Hakuna mtu atapata upendeleo kwa sababu alimuunga Lissu mkono na Heche, tutachagua watu kutokana na uwezo, uwezo wako utakuweka kwenye nafasi tulihubiri mabadiliko na tutasimamia mabadiliko hakuna mtu ataonewa kwa sababu hakutuunga mkono kuweni na amani kabisa."