Jumamosi , 7th Apr , 2018

Timu Yanga SC itashuka dimbani alasiri ya leo kuvaana na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wake kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika huku ikiwa inawakosa baadhi ya wachezaji wake.

Katika mchezo huo, Yanga itawakosa wachezaji wote wa kikosi cha kwanza, mabeki Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Obrey Chirwa ambao wote walionyeshwa kadi za njano katika mechi mbili zilizopita za nyumbani na ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Kwa upande wake, Welaita Ditcha nao watawakosa wachezaji wao wawili, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Zamalek ya Misri, wakati kocha Msaidizi wa Yanga Mzambia Noel Mwandila naye hataruhusiwa kukaa benchi leo, ingawa aliyotolewa Gaborone alikuwa Kocha Msaidizi mwingine, Nsajigwa Shadrack.

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo na mara ya nne kihistoria kwa timu ya Yanga kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.