Semina ya siku mbili kwa waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa ngazi ya juu nchini (elite) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu inaanza kesho kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Waamuzi na waamuzi wasaidizi 22 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki katika semina hiyo, ambayo pia itahusisha mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test), na itamalizika keshokutwa Machi 16 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Afisa Habari wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, ambapo pia amezungumzia ligi kuu ya soka Tanzania bara ambayo itaendelea kesho kwa michezo mitatu kupigwa katika viwanja tofauti hapa nchini ambapo mabingwa watetezi Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam wanaikaribisha Coastal Union ya Tanga katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.
