Alhamisi , 7th Mei , 2015

Timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa wavu wa ufukweni inatarajia kushuka dimbani hapo kesho kuumana na Rwanda katika mchezo wa mashindano ya kanda ya tano yaliyoanza kutimua vumbi leo jijini Mombasa Kenya.

Akizungumza na East Africa Radio, katibu mkuu wa chama cha mpira wa wavu nchini TAVA, Allen Alex amesema, ana imani kuwa timu hiyo itafanya vizuri kutokana na kuundwa na wachezaji wenye kiwango kizuri.

Alex amesema, mpaka sasa matumaini ya Tanzania kuendelea mbele kupitia mpira wa wavu yamebakia kwa timu ya wanawake baada ya timu ya wanaume kuondolewa katika hatua za awali.

Katika michuano hiyo, Timu mbili zitakazofanya vizuri zitafuzu kuingia hatua ya pili na kukutana na timu kutoka kanda ya sita ili kupata nchi nne zitakazofuzu kushiriki michuano ya Afrika itakayofanyika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu nchini Congo Brazzaville.