Alhamisi , 1st Nov , 2018

Shirikisho la soka nchini Benin (FBF), limeridhia wachezaji 10 wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 kwenda jela miezi 10 baada ya kufanya udanganyifu wa umri wakati wa michuano ya kuwania kufuzu AFCON ya vijana 2019.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Benin chini ya miaka 17.

Wachezaji hao wamehukumiwa kwenda jela miezi 10 ikiwa ni mwezi mmoja kwa kila mtu pamoja na  rais wa zamani wa Shirikisho la soka nchini humo, Anjorin Moucharafou ambaye yeye amehukumiwa miezi 2 jela kwa kushiriki katika udanganyifu huo.

Maamuzi hayo yamefanyika katika mahakama ya Cotonou baada ya vijana hao kukutwa na hatia kwa kufanya udanganyifu kwenye timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ambapo vipimo vya MRI, vilibaini wachezaji hao wa Benin walikua wamedanganya umri.

Wachezaji hao 10 wa Benin walibainika kudanganya umri nchini Niger, mwezi Septemba mwaka huu,  walipokwenda kushiriki michezo ya awali ya kuwania kufuzu michuano ya Afrika ya vijana chini ya miaka 17 itakayofanyika hapa nchini Tanzania mwaka 2019.

Uamuzi huo wa mahakama umekuja baada ya timu hiyo kuondolewa katika michuano hiyo ambapo tangu warejee nchini humo wakitokea Niger wachezaji hao na rais huyo wa zamani walishikiliwa na polisi na kukaa rumande hadi hukumu ilipotolewa jana.

Hii sio mara ya kwanza kwa Benin kukutwa na hatia na kufungiwa na mamlaka za juu za soka ikiwamo CAF na FIFA. Ilikutwa na tatizo hilo la kudanganya umri katika miaka ya 2016, 2010, 2012 na 2004.