Ijumaa , 25th Jul , 2014

Rais wa shirikisho la soka nchini TFF Jamal Malinzi ametoa wito kwa shule za msingi, sekondari na vyuo kuhakikisha wanaanzisha mitaala ya michezo katika masomo yao hasa katika kufundisha waamuzi kwani ndio tatizo kubwa kwa sasa nchini

Baadhi ya waamuzi wakiwa katika kozi ya uamuzi ya FIFA.

Waamuzi 30 wa Tanzania wamehitimu kozi ya uamuzi wa FIFA na kukabidhiwa vyeti vyao na Rais wa TFF, Jamal Malinzi ambaye hii leo ndiye amefunga kozi hiyo iliyokuwa ikifanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam

Malinzi amesema ni wakati sasa kwa vijana kujitokeza katika mafunzo ya waamuzi na pia ametoa wito kwa mashule hasa vyuo kuwa na mafunzo ya waamuzi katika mitaala yao ili kupata waamuzi bora na wasomi na hivyo kuongeza idadi ya waamuzi wa soka hapa nchini

Kozi hiyo ya siku 5 ambayo ilianza Julai 21 mwaka huu iliendeshwa na mkufunzi wa FIFA kanda ya nchi za kusini mwa Afrika Carlos Enriques ambaye amemuhakikishia Rais wa TFF Jamal Malinzi kuwa ategemee uamuzi bora katika mashindano mbalimbali yajayo

Naye Agnes Pantaleo ambaye ni moja kati ya waamuzi wachache wa kike waliohudhuria kozi hiyo amesema kozi hiyo imemfurahisha sana hasa baada ya kujifunza mambo mengi mapya na kubwa ni kwa washiriki wote kufaulu mitihani yao na ametoa wito kwa wanawake wengine kujitokeza kwa wingi katika kozi zijazo kwani fani ya uamuzi ni kama kazi nyingine.