VPL raundi ya 25 yaanza kwa sare

Alhamisi , 8th Apr , 2021

Michezo miwili ya ligi kuu soka Tanznaia bara raundi ya 25 imemaliza kwa timu kugawana alama, baada ya micho hiyo yote kumalizika kwa sare, Mchezo mmoja ulipigwa jijini mbeya na mwingine mkoani Lindi.

Wachezaji wakiwania mpira kwenye moja ya mchezo wa ligi kuu Tanznaia bara

Mchezo wa mapema ulianza kutimua vumbi majaira ya Saa 8:00 mchana, mchezo ambao ulipigwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya ambapo timu kizazi kipya Mbeya City walikuwa wenyeji wa kagera Sugar na mchezo huo ukamalizika kwa sare ya bila kufungana 0-0.

Baada ya timu hizi kugawana alama moja moja sasa mbeya City wanafikisha alama 21 kwenye michezo 25 na wanasalia nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi, Kagera Sugar wanasalia nafasi ya 13 na kwa matokeo haya wanafikisha alama 26 kwenye michezo 25.

Mchezo mwingine ulipigwa mjini Lwangwa mkoani Lindi katika uwanja wa Majaliwa ambapo Namungo FC walikuwa wenyeji wa Ihefu FC na mchezo huo umemalizika kwa sare ya bao 1-1, Ihefu ndio walikuwa wa kwanza kufunga bao dakika ya 23 kupitia kwa Raphael Daud, lakini baadae kipindi cha pili dakika ya 61 Ibrahim Mkoko akaisawazishia Namungo fc.

Namungo wanafikisha alama 28 wakiwa nafasi ya 10 na mchezo wa leo ni mchezo wao wa 19, Ihefu wanafikisha alama 21 na wapo nafasi ya 17 na mchezo wa leo ulikuwa wa 25.