Alhamisi , 28th Jul , 2016

Viongozi wa soka la vijana nchini wametakiwa kujua na kuzingatia kanuni ili za soka katika mchezo husika ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mashindano.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu shiriki za mashindano ya vijana Airtel Rising Stars, katibu mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF Celestine Mwesigwa amesema, kila shindano linakanuni zake hivyo viongozi wa benchi la ufundi wanalazimika kujua kanuni na kuzifundisha kuanzia kwa vijana.

Mwesigwa amesema, viongozi wanatakiwa kuzijua kwa umakini kanuni za kila mchezo kwani iwapo watakosea kunauwezekano mkubwa wa kupoteza matokeo hata kama timu shiriki itakuwa ni nzuri.

Mwesigwa amewataka pia wazazi kutoa sapoti kwa vijana ambao wanashiriki mashindano hayo ili waweze kufanya vizuri zaidi na kukuza soka kwa upande wao ambapo pia litakuwa na faida hapo baadae kwa kuwapatia ajira.

Mwesigwa amasema, viongozi wa vilabu pia wanawajibu wa kufuatilia mashindano hayo ili kuweza kupata vijana ambao watawasaidia katika mashindano mbalimbali pamoja na kuepusha gharama za kununua wachezaji kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuvitumikia vilabu vyao.

Mashindano ya Airtel Rising Stars yanatarajiwa kuanza rasmi Julai 31 mwaka huu kwa kushirikisha timu za Mbeya, Ilala, Temeke, Kinondoni, Mwanza na Morogoro kwa upande wa wavulana huku kwa upande wa wasichana yakishirikisha mikoa ya Lindi, Zanzibar, Arusha, Ilala, Temeke na Kinondoni.