Cristiano Ronaldo akihuzunika baada ya timu yake kuondolewa kwenye michuano ya UEFA EUROS kwenye hatua ya 16 bora baada ya kufungwa 1-0 dhidi ya Ubelgiji usiku wa jana.
6 - Ni idadi ya awamu ya michuano ya UEFA EUROS ambayo nyota wa Ureno CR7 huenda akaikosa kutokana na michuano hiyo kutaraji kufanyika mwaka 2025 muda ambao nyota huyo anatazamiwa kuwa na miaka 40 hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kutundika daruga kabla ya umri huo kufika na kuikosa michuano hiyo ambayo tayari ameichezea kwa awamu 5.
5 – Ni idadi ya wajumbe waliopitishwa na mkutano mkuu wa klabu ya Yanga uliofanyika Jumapili ya jana Juni 27, 2021 Chang'ombe jijini Dar es Salaam ili kuunda baraza jipya la wadhamini wa klabu hiyo, wajumbe hao ni George Mkuchika, Geofrey Mwambe, Abbas Tarimba, Mama Fatma Karume na Mwigulu Nchemba.
Mbali na majina hayo, mkutano huo pia ulipitisha mapendekezo ya mabadiliko ya katiba mpya inayowezesha klabu hiyo kwenda kwenye mfumo mpya wa mabadiliko ya uendweshaji wa klabu huku wafadhili wa klabu hiyo GSM waliahidi kushiriki kwenye ujenzi wa kituo cha mazoezi cha kisasa kitakachokuwa na mabweni, mabwawa ya kuongelea na miundo mbinu mingi ya kisasa.
4 – Ni idadi ya timu zilizofuzu kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya COPA AMERICA, bara la Amerika ya Kusini kutoka kila kundi B, Brazil imefuzu ikiwa kinara wa kundi hilo akiwa na alama 10 baada ya usiku wa kuamkia leo kutoa sare ya 1-1 kwa bao la Eder Militao dk37, Angel Mena akiwafungia Ecuardo dk 53 na kuwafanya Ecuardo kufika alama 3 na kumaliza nafasi ya nne.
Peru imefuzu baada ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Venezuela bao pekee lililofungwa na Andre Carrilo dk43 na kuwafanya Peru kufikisha alama 7 na kushika nafasi ya pili ilhali Colombia wakiwa watatu kwa jumla ya alama 4 na Venezuela kuwa kibonde kwa kuburuza mkia akiwa na alama mbili.
3 - Ni jumla ya mabao yaliyofungwa usiku wa kuamkia leo kwenye michezo miwili ya hatua ya 16 bora ya michuano ya UEFA EUROS, Czech iliifunga Uholanzi 2-0 mabao yaliyofungwa na Thomas Holes dk68 na Patrick Schick dk80 wakati Ubelgiji imeivua ubingwa ureno kwa kuifunga 1-0 bao pekee la Thorgan Hazard dk42.
Kwa matokeo hayo, Czech itacheza vs Denmark ilhali Italy itakipiga na Ubelgiji kwenye robo fainali tarehe 3 July 2021.
Hatua ya 16 bora ya michuano hiyo itaendelea usiku wa leo kwa michezo 2, Croatia vs Spain saa 1:00 usiku, Ufaransa vs Swizz saa 4:00 usiku.
2 – Ni idadi ya timu zilizoshuka dimbani kwenye ligi ya kikapu nchini Marekani NBA, ambapo timu ya Milwaukee Bucks imefanikiwa kuibuka na ushindi wa alama 113-102 dhidi ya Atlanta Hawks kwenye mchezo wa mzunguko wa tatu wa fainali ya ligi hiyo kwa ukanda wa Mashariki na kuwafanya Bucks kuongoza jumla ya michezo miwili kwa mmoja.
Kris Middleton wa Bucks ndiye aliyeibuka kinara wa mchezo huo kwa kufikisha alama 38, rebaundi 11 na assisti 7 na kumpiku nyota wa Atlanta Trae Young aliyeambulia alama 35 na assisti 4 pekee. NBA inataraji kuendelea tena kesho kwa mchezo mmoja saa 10 Alfajiri ya kuamkia kesho ambapo Clippers watachuana na Phoenix Suns kwa upande wa fainali ya ukanda wa Magharibi.
1 – Ni nafasi ya ubora anayoshikilia mwanamama Johana Konta kwenye viwango vya mchezo wa tenisi nchini England ambaye usiku wakuamkia leo ameondolewa kwenye michuano mikubwa ya Tenis ya Gland slam itakayotimua vumbi kuanzia leo hii Juni 28, 2021 kutokana na nyota huyo kuwekwa karantini ya siku 10 baada ya kuwa karibu na mgonjwa wa Covid-19.

