Mfungaji wa bao pekee la Ureno dhidi ya Croatia kiungo Ricardo Quaresma.
Timu ya taifa ya Ureno jana usiku ilifanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Euro 2016 inayoendelea nchini Ufaransa baada ya kuilaza timu ngumu ya Croatia kwa bao 1-0 katika mchezo mkali mno wa hatua ya 16 bora mchezo uliodumu kwa dakika 120 ukipigwa katika dimba la Stade Bollaert- Delelis mjini Lens.
Mshambuliaji hatari na nahodha wa Ureno Cristiano Ronaldo alipika bao hilo muhimu katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Carlos Velasco raia wa Hispania katika dakika 30 za nyongeza baada ya awali mchezo huo kumalizika kwa suluhu ya 0-0 katika dakika 90 za kawaida.
Bao la ushindi la Ureno ambayo imeonekana imekuwa na mwendo wa kusuasua katika michuano hiyo pamoja na kuendelea kuvuka kwenda hatua za mbele zaidi lilifungwa kunako dakika ya 117 kwa kichwa baada ya kiungo mkongwe Ricardo Quaresma kuuwahi mpira uliokuwa unaelea karibu na goli la Croatia kufuatia shuti kali la Ronaldo kutemwa na kipa Danijel Subasic na mfungaji huyo aliyeingia kipindi cha pili dakika ya 87 kuchukua nafasi ya Joao Mario.
Ronaldo ambaye muda wote wa mchezo huo alionekana kukabwa kila eneo na walinzi wawili wawili wa Croatia pamoja na kuonekana kutong'aa sana katika mchezo huo lakini kazi yake hiyo ya kupika bao hilo moja ilipongezwa na wachezaji wenzake na mashabiki.
Na kwa matokeo hayo Ureno ambayo mchezo huo wa jana usiku ndiyo ulikuwa ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo msimu huu sasa itavaana na timu isiyotabirika ya Poland katika hatua ya robo fainali.