Jumamosi , 19th Mar , 2016

Twiga Stars iliondoka jana usiku saa nne kuelekea nchini Zimbabwe na kuwasili salama mjini Harare ambako kesho itashuka dimbani kuvaana na timu ya wanawake ya huko katika mchezo wa marudiano ambao watanzania wengi hivi sasa wanaiombea timu ushindi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja akimkabidhi bendera Nahodha wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu , Asha Rashidi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja amewataka Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake kuwapa raha watanzania kwa kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa marudiano na Timu ya Taifa ya Wanawake ya Zimbabwe inayotarajiwa kuchezwa Jumapili Machi 20.

Akiongea wakati wa zoezi la kuikabidhi bendera timu hiyo jana tarehe 18 Machi , 2016 lililofanyika katika Ofisi za TFF Jijini Dar es Salaam, alieleza kuwa watanzania wanayo imani kubwa na timu hiyo hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

“Mnapoondoka kuelekea Zimbabwe mwende mkifikiria mambo matatu, kuitendea haki nchi yenu, kuutendea haki mpira na kuitendea haki Timu ya Taifa ya Wanawake Kwenye mchezo wenu wachezaji lazima mpendane, mcheze kwa kutumia nguvu na mfikirie kuiletea nchi sifa.” alisema Kiganja.

Kwa upande wake Kocha wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa miguu Nasra Mohamed alibainisha kuwa, wachezaji wameandaliwa vyema na mahitaji yao yote yako kamili .

“Timu yangu ushindi wa ugenini ni muhimu sana na tayari tumeshayafanyia marekebisho makosa yaliyojitoleza katika mchezo wetu wa awali hivyo wachezaji wangu wameandaliwa vyema kiufundi na kisaikolojia kwa ajili ya kuwapa raha watanzaniai” alisema Mohamed

Timu hiyo imeondoka na wachezaji 19, pamoja na Viongozi sita. Ikiwa na kumbukumbu za kupoteza mchezo wa awali kwa kufungwa goli 2 dhidi ya goli 1, katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.