Jumanne , 15th Sep , 2015

Tanzania na Ethiopia zimefanikiwa katika kuepusha wasichana kuozwa na badala yake wanaendelea na masomo kutokana na mikakati kadhaa iliyotumika ikiwemo kushirikisha jamii katika mijadala kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wake wa Marais na Wakuu wa nchi za Afrika mara baada ya kikao cha kampeni ya kutokomeza ndoa za utotoni

Princess Mabel Van Oranje muasisi na mwenyekiti wa ubia wa kimataifa wa kumaliza ndoa za utotoni amesema hayo wakati wa mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuhusu harakati hizo.

Akinukuu ripoti ya baraza la idadi ya watu duniani, Princess Oranje ametaja mkakati mwingine kuwa ni kuwapatia wasichana mbinu mbadala za kujiinua kiuchumi, kuhakikisha wana sare za shule na mahitaji yote ya shuleni, lakini pia mijadala hii ya kijamii imeleta tofauti kubwa.

Katika utafiti huo baraza la idadi ya watu duniani lilibaini kuwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 17 ambao walipatiwa mbuzi ili wasiolewe na badala yake wasalie shuleni walikuwa na nafasi ya theluthi mbili zaidi kuendelea na masomo kuliko wale ambao hawakupatiwa miradi hiyo.