Jumapili , 19th Nov , 2023

Serikali kupitia Wizara ya Madini imesema inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara na ina mipango ya muda mrefu na muda mfupi wa  kuzitatua changamoto hizo.

Waziri Mavunde akizungumza na wachimbaji wadogo Mererani

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Anthony mavunde, wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite , wafanyabiashara na wamiliki wa vitalu vya uchimbaji madini katika mkutano maalum ulioitishwa na Serikali ili kujadili changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

Mapema baada ya Mkuu wa Mkoa wa  Manyara Mh. Queen Sendiga kutoa taarifa , wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya Tanzanite walielezea juu ya changamoto walizonazo ikiwa pamoja na ukosefu wa nishati ya umeme katika migodi, mitobozano chini ya ardhi, ubovu wa miundombinu ya barabara, kukosekana kwa minada ya kuuza madini, ukosefu wa maji na vituo vya afya, ukosefu wa mitaji ya kuendeleza uchimbaji na vifaa duni vya uchimbaji.

Akielezea kuhusu mikakati iliyopo ya kutatua changamoto hizo Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupitia upya kanuni za masoko, uongezaji thamani na kanuni za  eneo tengefu la Mererani ili kufanikisha minada ya vito pasipo vikwazo.

Kuhusu Mitobozano Waziri Mavunde amesema hakuna sheria inayoruhusu mitobozano katika uchimbaji madini kisheria leseni zote zina mipaka hivyo kila mchimbaji azingatie mipaka yake iliyopo katika leseni na kumtaka Afisa Madini Mkazi wa Mirerani kuhakiksha anakaa na wadau kutatua changamoto ili kuruhusu shughuli za madini ziendelee pasipo kuleta athari katika ukuaji wa sekta.