Jumanne , 17th Mei , 2022

Uongozi wa klabu ya Simba umekiri kosa na kubainisha kuwa ipo tayari kulipa faini ambayo Bodi ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imewatoza.

kikosi cha Simba.

Jana CAF ilieleza kuitoza klabu hiyo faini ya Sh23 Milioni kwa kosa la kuwasha moto eneo la katikati ya uwanja wakati wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kusali.

Picha za tukio hilo zilisambaa wakati wa mchezo wa marudiano wa robo fainali ya CAF nchini Afrika Kusini, Simba ilipocheza na wenyeji, Orlando Pirates.

Katika mchezo huo, Simba ilifungwa bao 1-0 na kuondoshwa kwa mikwaju ya penalti kufuatia ushindi wa bao 1-0 ilioupata awali nyumbani kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku wenyeji wakitinga nusu fainali.

Kauli hiyo imesemwa na Mkurungezi wa kitengo cha habari wa Simba, Ahmed Ally amesema hawana cha kujitetea kwenye adhabu hiyo, ni kosa walifanya hivyo hawana budi kulipa faini hiyo.

'Taarifa za adhabu hiyo tunazo na hatuna budi kulipa faini kwa kuwa ni kosa ambalo limeshafanyika na CAF imetoa adhabu yake," amesema Ahmed.