Jumapili , 17th Apr , 2016

Timu ya soka ya wekundu wa Msimbazi Simba wameendelea kuwa wateja wa timu ya Toto Africans baada ya hii leo kushindwa kupata matokeo mbele ya timu hiyo maarufu kama wanakishimapanda kutoka jijini Mwanza katika mchezo muhimu kwa timu zote mbili.

Wachezaji wa Simba wakiwapungia mashabiki wa timu hiyo baada ya mchezo wao dhidi ya Toto hii leo.

Ikiwatumia baadhi ya wachezaji chipukizi na wenye vipaji waliowahi kuwika na Simba kama Edward Christopher, Hassan Khatib na Abdallah Seseme wameweza kucheza vema na kuisaidia Toto kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Goli pekee la wanakishamapanda Toto Africans limefungwa kunako dakika ya 20 na mfungaji hatari wa timu hiyo kwa sasa Waziri Junior baada ya kupiga shuti kali nje ya 18 lililomshinda kipa mu-Ivory Coast Vicent Agban na kujaa wavuni moja kwa moja na kuipa alama tatu muhimu timu ya Toto ambayo sasa imefikisha alama 30 kwa michezo 27.

Simba ambayo imekuwa ikipata tabu mara kwa mara kwa misimu kadhaa kila inapokutana na vijana hao wa Toto ambao kwa sasa wananolewa na kocha John Tegete akisaidiwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars Rogasian Kaijage ilishuhudia kocha wake Mganda Jackson Mayanja akitolewa nje kwenye benchi na mwamuzi Ahmada kutokana na kinachoonekana kupishana kauli, hivyo Simba ikawa chini ya uangalizi wa kocha wa Makipa Adam Abdallah.

Pigo lingine kwa Simba lilikuwa mwanzoni mwa kipindi cha pili pale iliposhuhudia beki wake kisiki wa upande wa kulia Hassan Kessy akipewa kadi nyekundu na hivyo kuivuruga kabisa timu hiyo ambayo hii leo ilikosa kabisa mbinu mbadala za kuipenya ngome ngumu iliyocheza kwa nidhamu kubwa dakika zote za mchezo huo ikiongozwa na beki kisiki wa kati Hassan Khatib aliyewahi kuwika na Simba kabla ya kutupiwa virago msimu huu mwanzoni.

Kessy ambaye hii leo alianza vema mchezo huo huku akipandisha mashambulizi kwa kasi mara kwa mara katika lango la Toto alitolewa nje baada ya kumchezea faulo mbaya, mshambuliaji kinda wa zamani wa Simba Edward Christopher kunako dakika ya 2 kipini cha pili.

Matokeo haya yanaifanya Simba ambayo inahaha kusaka nafasi ya ushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kubaki katika nafasi ya pili kwa alama zao 57 mbili nyuma ya vinara Yanga ambao wako nyuma kwa mchezo mmoja huku Simba wakifikisha michezo 25.

Kwa misimu kadhaa sasa timu ya soka ya Simba imekuwa ikipata shida kila inapovaana na timu ya soka ya Toto Africans ya Mwanza katika michuano ya ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL ikishuhudiwa Simba ikipotea ama kuambulia sare mbele ya timu hiyo.