Jumatano , 26th Aug , 2015

Timu sita shiriki za michuano ya All Africa Games zinatarajiwa kuanza kuondoka nchini Agosti 30 mwaka huu kuelekea nchini Congo Brazzaville kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba nne mwaka huu.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Baraza la Michezo Nchini BMT Najaha Bakari amesema, kila timu shiriki itaondoka nchini kutokana na ratiba ya michuano yao huku kila timu ikiondoka na kiongozi mmoja kwa kila timu isipokuwa timu ya mpira wa miguu wanawake ambapo wataondoka wakiwa 23 ikijumuishwa na viongozi wa timu.

Najaha amesema timu ya ngumi ya taifa itaondoka Agosti 30 ikiwa na msafara wa mabondia watatu, huku timu ya mpira wa miguu ya wanawake Twiga Stars wakiwa 23 pamoja na viongozi wakiongozana na wanaoshiriki mashindano ya kuogelea wawili wakiondoka Septemba Mosi mwaka huu.

Najaha amesema, timu ya tenisi walemavu wakiwa wawili, riadha watatu na judo wawili wataondoka nchini Septemba 11 mwaka huu.