Jumatano , 6th Feb , 2019

Shirikisho la soka nchini (TFF), limesisitiza kuwa hakutokuwa na mabadiliko ya tarehe ya mchezo wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga utapigwa siku ile ile iliyopangwa awali ya Februari 16, 2019.

Vikosi vya Simba na Yanga

Kupitia taarifa yake leo TFF imeeleza kuwa hakuna mabadiliko yoyote katika mchezo huo na kwamba utapigwa katika uwanja wa taifa.

''Mchezo wa ligi kuu namba 270 kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Simba utachezwa kama ulivyopangwa'', imeeleza taarifa hiyo ambayo imetoka siku moja tu tangu klabu ya Yanga ilalamikie upangaji wa ratiba.

Kumekuwa na tetesi nyingi kuwa huenda mchezo huo ukabadilishiwa tarehe kutokana na Simba kuwa na mchezo wa Ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly Jumanne ya Februari 12.

Yanga nayo imelalamika kuwa ratiba ya ligi imekuwa haiwasaidii wachezaji wao kutokana na kulazimika kusafiri kwa kilometa zaidi ya 15 kutoka Tanga hadi Singida kisha kurudi Tanga kwaajili ya mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania.