Moja ya wachezaji wa mchezo wa tenisi kwa walemavu akifanya mazoezi jijini Dar es Salaam.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya mchezo wa tenisi kwa walemavu ya Tanzania [wheel chair tenis] Riziki Salumu amesema timu hiyo ambayo imekuwa ikifanya vema katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi inahitaji kuungwa mkono hasa katika upande wa vifaa.
Riziki amesema pamoja na kufanya maandalizi kwa muda mrefu timu hiyo imekuwa ikikosa ufanisi hasa kutokana na ukosefu wa baiskeli za magurudumu [wheel chair] ambazo ndiyo muhimu katika mchezo huo kwa walemavu.
Aidha Riziki amesema pamoja na kikosi hicho kuwa ni moja ya timu tatu bora katika mchezo huo barani Afrika na namba moja kwa nchi za Afrika Mashariki na kati wamekuwa wakikwama katika mashindano mbalimbali ya kimataifa hasa kutokana na kutumia vifaa vilivyochaakaa na kupitwa na wakati kama baiskeli za kuchezea [Wheel chair] ambazo haziendani na kasi ya mchezo ukilinganisha na wanazotumia wachezaji toka mataifa mengine kama Afrika kusini.
Huku ikitumia vifaa vya zamani timu hiyo kwa sasa imeshaanza maandalizi ya mapema yakujiwinda na michuano mikubwa miwili ya kimataifa itakayofanyika mwishoni mwa mwaka huu ikiwemo ile ya MBP Palibas na ile ya kufuzu kwa fainali za michuano ya dunia.
Mwisho Riziki amesema changamoto kubwa inayohitaji utatuzi wa haraka ni viti vya magurudumu ama baiskeli za kuchezea wheel chair ambazo kwa wachezaji hao ndio kama miguu yao ya kuchezea ambapo bila hiyo hawawezi kucheza.