Riziki Salum kocha wa timu ya taifa ya tenisi ya walemavu ya Tanzania.
Riziki Salum amesema iwapo kama Serikali itaamua moja kwa moja kwakushirikiana na wadau mbalimbali yakiwepo makampuni na kutoa sapoti ya kutosha kwa mchezo huo wanaimani kubwa kuwa wataweza kufanya vema katika michuano mbalimbali inayowakabili na kuipeperusha vema bendera ya taifa ndani na nje ya mipaka katika medani ya kimataifa.
Timu hiyo ya taifa imeweza kutetea ubingwa wake kwa mara nyingine wa michuano ya wazi ya Kenya iliyopigwa hivi karibuni jijini Nairobi.
Salum amesema pamoja na kuibuka na ubingwa huo kwa upande wa wanawake na wanaume lakini katika maandalizi yao yaliyopita walikuwa wakifanya katika mazingira magumu na yakukatisha tamaa katika hali ngumu sana hasa kutokana na kukosa vifaa vya kutosha vya kisasa, huduma za matibabu pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa wachezaji kama nauli na posho zingine.
Aidha Salum amesema ni vema sasa ifike wakati wadau na hasa Serikali kuwaangalia vijana hasa kama hao walemavu wa timu ya tenisi ambao wanajitolea kwa moyo wao na kuitangaza vema nchi kimataifa na kuwapa misaada ya kutosha hata kuwatafutia udhamini ili wafanye maandalizi bora na yakutosha na waweze kufanya vema zaidi ya walipofikia.
Akimalizia Salum amesisitiza kuwa ni vema ikatokea taasisi au Serikali ikabeba majukumu ya timu na kuiwezesha kuwa bora na ikafanya mambo makubwa zaidi kimataifa na kimsingi amesema kitendo cha kutwaa ubingwa huo, kunaashiria Tanzania ipo vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye mchezo wa tenisi kwa wachezaji wenye ulemavu ama mahitaji maalumu hivyo ni wazi wanahitaji kuwezeshwa kwakuwa wameshaonyesha wanaweza.