Jumamosi , 9th Apr , 2016

Wakati sakata la rushwa na upangaji wa matokeo ya michezo miwili ya ligi daraja la kwanza kundi C likiendelea kushika kasi huku wadau wa soka wakimkomalia Rais wa TFF Jamal Malinzi wakimtaka ajiuzuru wadhifa wake tayari TAKUKURU wamepiga kambi TFF.

Jengo la ofisi za makao makuu ya shirikisho la soka nchini TFF lililoko maeneo ya Karume Ilala jijini Dar es Salaam.

Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) tayari imeanza uchunguzi kuhusu tuhuma za rushwa katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kunaswa kwa sauti zinazohisiwa kuwa ni za Maofisa na viongozi wa waandamizi ama wa juu wa TFF wakipanga matokeo ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Geita Gold Sports na JKT Kanembwa.

Shirikisho hilo, tayari limemsimamisha kazi msaidizi wa Rais, Juma Matandika huku Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Martin Chacha akitangaza kujiuzulu nafasi yake.

Ofisa Habari wa Takukuru, Tunu Mlei amesema kutokana na kuanza kwa uchunguzi huo hivyo kisheria suala hilo kwa hivi sasa hawaruhusiwi kulizungumzia na wataliweka wazi mara baada ya uchunguzi kukamilika.

“Takukuru tayari imeanza uchunguzi wa hizo tuhuma za rushwa inayodhaniwa TFF inahusika moja kwa moja, hivyo hilo suala lipo kwetu na linashughulikiwa kisheria haturuhusiwi kulizungumza hadi pale litakapokamilika, hivyo tunawaomba wadau wa soka kuwa wavumilivu katika kipindi hiki tukisubiria uchunguzi huo utakapomalizika,” amesema Mlei.

Sakata hilo la upangaji wa matokeo ya michezo hiyo ya mwisho ya ligi daraja la kwanza kutoka kundi C pamoja na mchezo kati ya wenyeji JKT Kanembwa ambayo ilipigwa bao 8-0 na Geita Gold Sports pia inahusisha mchezo baina ya maafande wa Polisi Tabora walioibuka na ushindi wa bao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro ambapo michezo hiyo yote ilimalizika kwa zaidi ya dakika mia 100 tofauti kabisa na muda wa kawaida wa mchezo wa dakika 90 na hivyo kuzua sintofahamu na kupelekea TFF kupeleka malalamiko kwenye kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo ambayo nayo ilitoa adhabu kwa wale waliokutwa na hatia.