Jumamosi , 7th Jul , 2018

Singida United ambayo ilimaliza katika nafasi ya 5 katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi kuu soka Tanzania Bara 2017/18, imeendelea kuimarisha kikosi chake, mara hii ikimpa changamoto mlinda mlango wake namba moja Manyika Jr kwa kumsajili aliyekuwa kipa wa Njombe Mji David Kissu.

Mlinda mlango wa Singida United Peter Manyika Jr.

Timu hiyo ambayo tayari imeshafanya usajili wa nafasi kadhaa za ndani, imenasa sahihi ya David Kissu golikipa ambaye msimu uliopita aliichezea klabu ya Njombe Mji na alionekana kufanya vizuri licha ya timu yake kushuka daraja lakini alionekana hodari kwa upande wake.

Kissu ametua Singida United kwa Kandarasi ya miaka mitatu hivyo ataungana na makipa wengine akiwemo namba moja Peter Manyika Jr na Ally Mustapha ambaye ni kipa namba mbili.

Kushoto ni David Kissu mchezaji mpya wa Singida United akikabidhiwa jezi na Mkurugenzi wa timu Festo Sanga.

Mkataba wa mlinda mlango huyo ndani ya Singida United utamalizika mwaka 2021. Mkurugenzi wa timu Festo Sanga amesema lengo la kuongeza mlinda mlango mwenye uzoefu ni kuhakikisha timu hiyo inakuwa na kikosi kipana ili kushindania ubingwa msimu wa 2018/19.

''Ni kweli tumemsajili na kumtambulisha David Kissu ambaye alionesha kiwango kikubwa akiwa na Njombe Mji msimu uliopita tunaamini atasaidia timu kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu ujao na hilo ndio lengo letu la kuwa na kikosi kipana'', amesema Sanga.