Jumatano , 28th Nov , 2018

Klabu ya Singida United imefanikiwa kuwanasa makinda wawili kutoka nchini Zambia, Jonathan Daka na Gift Chikwangala kwaajili ya kuimarisha kikosi chake kuelekea mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara.

Wachezaji wapya wa Singida United, Jonathan Daka (kushoto) na Gift Chikwangala (kulia)

Gifti Chikwangala anayecheza nafasi ya ushambuliaji, ameingia kandarasi ya kuitumikia Singida United kwa mkataba wa miaka mitatu (3).

Kwa upande wa Jonathan Daka (20) ambaye anacheza katika timu ya taifa ya vijana U-23 ya Zambia, Singida United imeingia naye mkataba wa miaka mitatu (3) ambapo taarifa rasmi ya Singida United imesema kuwa usajili wa wachezaji hao ni kuimarisha kikosi chake kuelekea michuano ya Sportpesa.

Katika miezi ya karibuni, Singida United imekuwa ikilaumiwa juu ya kutolipa stahiki kwa wachezaji wake jambo ambalo linapelekea wachezaji wengi kuachana na klabu hiyo. Uongozi wa klabu hiyo pia umethibitisha mara kadhaa juu ya kushuka kwa hali ya kiuchumi kuwa ndiyo sababu inayopelekea kuwepo kwa matatizo hayo.

Singida United inashikilia nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara, ikiwa na alama 18 baada ya kushuka dimbani michezo 14 mpaka sasa.