Jumatatu , 5th Dec , 2016

Klabu ya Simba ya Dar es Salaam inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania Bara 'imenyoosha mikono' na kukubali kukaa meza moja na baraza la wadhamini la klabu hiyo kabla ya mkutano mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 11, mwaka huu.

Haji Manara

 

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo Haji Manara amesema klabu hiyo imeamua kukubali ombi la baraza hilo, ili kuweka mambo sawa kuelekea mkutano huo na kutoa ufafanuzi kwa jambo lolote ambalo litakuwa halijaeleweka kuelekea katika mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa timu hiyo.

Manara amesema kuwa kikao hichokimepangwa kufanyika wakati wowote kati ya leo au kesho, na kwamba uongozi una imani kubwa kwamba wataelewana, huku akisisitiza kuwa mkutano mkuu wa klabu hiyo uko palepale, na tayari maandalizi yamekamilika.

Katibu wa Baraza la Bodi la Wadhamini wa Simba, Hamisi Kilomoni (katikati) akizungumza na wanahabari wiki iliyopita

Wiki iliyopita baraza hilo la wadhamini la Simba lilizungumza na wanahabari na kueleza malalamiko yake kuhusu mchakato wa mabadiliko ndani ya klabu hiyo, ambapo mwenyekiti wake Mzee Hamis Kilomoni alidai kuwa Baraza hilo haljashirikishwa katika hatua yoyote ikiwa ni pamoja na mkutano huo wa dharura, na kutishia kuuzuia endapo viongozi wa Simba hawatazungumza na wajumbe wa baraza hilo.