Ijumaa , 9th Oct , 2020

Simba SC, Yanga SC na Azam FC zimeendeleza ubora kwenye michezo ya ligi kuu Tanzania bara msimu huu, na ndio timu pekee ambazo hazijapoteza mchezo hata mmoja mpaka raundi ya tano ilipokamilika.

Simba SC ndio timu iliyofunga magoli mengi ligi kuu Tanzania bara msimu huu magoli 14 katika michezo 5

Ligi hiyo imefika raundi ya 5 na baada ya kumalizika kwa kalenda ya kimataifa ya FIFA itarejea katika raundi ya 6 kuanzia Oktoba 14.

Wakati tukisubiria urejeo wa ligi hiyo baada ya mechi za kimataifa za kirafiki, ni vyema ukabaki na kumbukumbu ya idadi ya michezo iliyopigwa ambayo ni 45.

Kipenga ikaona pia ni vyema ukakusogezea takwimu baada ya michezo ya raundi ya tano kukamilika.

Katika michezo 5 ambayo kila timu imecheza mpaka sasa ni timu 3 tu ambazo hazijafungwa mchezo hata mmoja,

Timu hizo ni Azam FC ambao wameshinda michezo yao yote na ndio vinara wa ligi wakiwa na alama 15, Simba SC wameshinda michezo 4 na wametoka sare mchezo mmoja wanajumla ya alama 13 wakiwa nafasi ya pili.

Timu nyingine ni Yanga nao hawajapoteza mchezo, wameshinda michezo 4 na wametoka sare mchezo mmoja wakiwa nafasi ya 3 na alama 13.

Azam FC ndio timu pekee iliyoshinda michezo yote 5 ya ligi kuu, na wanaongoza ligi wakiwa na alama 15

Ihefu na Mbeya City ndio timu zilizopoteza michezo mingi, 4 kila timu, na hawa Mbeya City ndo timu pekee ambayo haijashinda mchezo hata mmoja, ambapo katika michezo 5 wamefungwa michezo 4 na wametoka sare mchezo mmoja na wanaburuza mkia katika msimamo.

Ndugu zao Mbeya City ni Ihefu ambao wao wameshinda mchezo mmoja, wamefungwa michezo 4 wapo nafasi ya 17 na alama zao 3 kwenye msimamo.

Takwimu nyingine muhimu ni kwamba hadi tunakwenda mapumziko, Yamefungwa mabao 74 katika michezo hiyo 45 ambao ni wastani wa bao 1.644 kwa mchezo.

Mabingwa watetezi, Simba SC ndio timu iliyofunga mabao mengi, wamefunga jumla ya mabao 14 wakiwa na wastani wa kufunga goli 2.8 kwa mchezo, wakifuatiwa na Azam FC waliofunga mabao 9 na wastani wao wa kufunga kwa mchezo ni bao 1.8.

Klabu ya Manisapaa ya Kindondoni KMC wanashika nafasi ya tatu kwa kupachika mabao wakiwa wamefunga mara 8, na wastani wao wa kufunga kwa mchezo ni bao 1.6.

Timu iliyo katika nafasi ya 4 kufumania nyavu ni Yanga wenye wastani wa 1.4 kwa mchezo, kwani mpaka sasa wamefunga mabao 7 kwenye michezo 5.

Timu ya tano kucheka na nyavu ni Polisi Tanzania ambao wamefunga mabao 6 na wastani wao wa kufunga kwa mchezo ni 1.2.

JKT Tanzania ndio timu iliyofungwa mabao mengi ambayo ni 8, wakifuatiwa na Mbeya City na Ihefu ambao wote kwa pamoja wameruhusu mabao 7.

Simba ndio timu iliyokusanya alama nyingi katika viwanja vya ugenini katika michezo 3 ya ugenini ambapo wameshinda michezo 2 na wametoka sare mchezo mmoja, wamekusanya alama 7 kati ya 9.

Yanga na Azam FC zinafuatia huku zote zikiwa zimeshinda michezo miwili waliocheza ugenini, wamekusanya alama 6 kila timu.

Polisi Tanzania nayo imekusanya alama 6 katika michezo 3 ya ugenini, wameshinda michezo miwili na wamefungwa mchezo mmoja.

Azam FC, Biashara United, Simba SC na Dodoma Jiji Fc ndio timu zilizoshinda michezo yote waliocheza katika viwanja vyao vya nyumbani.