Wachezaji wa Simba Ibrahim Ajibu na Jamal Mnyate wakishangilia bao la kwanza.
Ushindi huo uliotokana na mabao ya Jamal Simba Mnyate mawili na mawili ya Shizza Ramadhani Kichuya, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 16, baada ya kucheza mechi sita, wakishinda tano na sare moja.
Baada ya ushindi huo, Simba inakwenda kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC Jumamosi wiki ijayo Uwanja huo huo wa Taifa.
Katika dimba Nangwanda Sijaona wanakuchele Ndanda Fc imewaangusha washindi wa Ngao ya Jamii Azam FC kwa mabao 2-1 na kuwafanya wanalambalamba hao kusalia na alama zao 10 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Mabao ya Ndanda yamefungwa na Riffat Khamis na Hajji Mponda, wakati la Azam FC lilifungwa na Nahodha John Raphael Bocco.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, JKT Ruvu wameshinda 2-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani, Prisons wametoka sare ya 0-0 na Mwadui Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Mbao FC Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Ligi hiyo inaendelea kesho kwa mechi mbili; Ruvu Shooting na Toto Africans Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani, Stand United na Yanga SC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na kesho kutwa African Lyon itamenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa.