Jumamosi , 16th Jan , 2016

Aliyekuwa Kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, amesema Simba imechelewa kumtimua Kocha Dylan Kerr kwani alianza muda mrefu kuitibua klabu hiyo.

Kerr ni kocha mzuri ila alishawaambia viongozi mapema kuwa hafai ndani ya timu kutokana na kutaka kufuata kile anachokiamini bila ya kushirikiana na wenzake hata kama anakosea.

Matola amesema, Simba imechelewa kumtimua kwani ameiweka timu mahali pabaya na kama angeondoka mapema klabu ingekuwa pazuri kwa hivi sasa.

Hivi karibuni Matola aliamua kuondoka mwenyewe Simba na kujiunga na Geita Gold Sports ya Ligi Daraja la Kwanza kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoelewana kwake na Kerr ambaye ni raia wa Uingereza.

Simba mapema wiki hii ilitangaza rasmi kuvunja mkataba na Kerr kwa kilichoelezwa kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi hicho katika mechi zake za michuano mbalimbali.