Kocha wa siku nyingi na mchambuzi wa soka nchini Tanzania Kenny Mwaisabula "Mzazi" amesema klabu ya Simba haipo makini katika kuchagua makocha sahihi na ndiyo maana inatimua makocha kila wakati.
Mwaisabula amesema ni kitu cha kushangaza kwa Simba kumfuta kazi Dylan Kerr wakati hadi sasa ameifikisha Simba nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara.
Mwaisabula ambaye aliwahi kuifundisha klabu ya soka ya Yanga, amesema Simba kuna tatizo la maamuzi ya kutafuta makocha, hivyo baadhi yao wanageukana pale mambo yanapoharibika na akaitaka ikae chini na kufikiria wapi wanakosea.
Uongozi wa Simba umeachana na kocha huyo baada ya miezi 6 ya mkataba wa mwaka mmoja na kuvunja huko mkataba ni makubaliano ya pande mbili.

