Ijumaa , 21st Sep , 2018

Wasiwasi uliokuwepo kuwa huenda Cristiano Ronaldo atakosa mchezo wa hatua ya makundi ya klabu bingwa Ulaya dhidi ya Man United sasa haupo baada ya kuepuka adhabu zaidi kutoka kwa UEFA.

Cristiano Ronaldo

Ndoto za nyota huyo kuendeleza historia nzuri katika michuano ya Ulaya hasa katika klabu yake mpya ya Juventus iliyeyuka baada ya kupata kadi nyekundu dakika ya 29, kwenye mchezo dhidi ya Valencia nchini Hispania, mchezo ambao Juventus ilishinda 2-0.

Kulikuwa na wasiwasi kuwa UEFA wangeweza kumuongezea adhabu nyota huyo baada ya kukiuka baadhi ya kanuni hasa ya kuchelewa uwanjani baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Sasa ataukosa mchezo mmoja pekee dhidi ya Young Boys utakaochezwa wiki mbili zijazo nchini Italia.

Man United itaikaribisha Juventus, 23 Oktoba katika uwanja wa Old Trafford, mchezo ambao Cristiano Ronaldo anatarajiwa kurejea katika klabu yake ya zamani akiwa na klabu ya pili tofauti baada ya kucheza akiwa na Real Madrid msimu wa 2012/13 .

Cristiano Ronaldo atarejea Old Trafford akiwa na klabu ya pili tofauti tangu alipoondoka mwaka 2009 baada ya kuichezea Man United michezo 196 na kuifungia mabao 84.

Matokeo rasmi ya hatua za kinidhamu zaidi zitakazochukuliwa dhidi ya mchezaji huyo hayatotajwa rasmi hadi hapo kamati ya maadili ya UEFA itakapokutana Alhamisi ya wiki ijayo, japokuwa taarifa mbalimbali zinaeleza kwamba tayari kamati hiyo imeshaangalia video ya tukio la kadi hiyo nyekundu na haina nia ya kuongeza adhabu zaidi kwa mchezaji huyo.