
Robert Pires akiwa ndani ya Studio za East Africa Radio.
Akiongea na www.eatv.tv mapema leo, Pires amesema Arsenal chini ya Unai Emery imekuwa timu imara jambo ambalo linamfanya kuamini kuwa katika mchezo wa kesho dhidi ya Liverpool washika bunduki hao wa London wataibuka na ushindi.
''Arsenal sasa imeimarika sana, inacheza kwa nguvu na kulazimisha kupata matokeo chanya, timu ya aina hii mara nyingi hushinda mechi zake na kutwaa ubingwa pia, naamini kesho Arsenal itashinda mabao 2-0'', amesema.
Pires mwenye miaka 45 yupo nchini, chini ya Barclays Tanzania kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni yao ya 'Superfans' utakaofanyika Mlimani City jijini Dar es salaam kesho Jumamosi Novemba 3, 2018.
Katika uzinduzi huo wa Super Fans Pires atakutana na mashabiki na kugawa zawadi mbalimbali ikiwemo fulana na mipira.
Akiwa na Asernal Pires alifanikiwa kushinda mataji mbalimbali ikiwemo FA mara mbili, EPL mara pili ukiwemo ule msimu wa 2003–04 ambao Arsenal ilishinda ubingwa bila ya kufungwa mchezo wowote.