Jumapili , 26th Aug , 2018

Rais wa shirikisho la mpira wa Kikapu nchini (TBF) Phares Magesa, ameeleza kufurahishwa na ushawishi mkubwa uliotengenezwa na michuano ya Sprite Bball Kings kwenye mchezo huo huku akiomba mashindano hayo yawepo tena mwakani.

Wachezaji wa Mchenga Bball Stars wakishangilia ubingwa wao

Magesa aliyasema hayo jana usiku wakati wa kukabidhi zawadi kwa mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2018, Mchenga Bball Stars, kwenye uwanja wa taifa wa ndani, ambapo alieleza kuwa mashindano hayo yamekuwa yakivutia watu wengi hivyo kuongeza thamani ya mchezo huo nchini.

''Kama tunavyoona watu wengi wamekuwa wakijaa uwanjani kushuhudia michuano hii, niombe tu wenzetu wa East Africa Television na Sprite ambao ndio waandaaji na wadhamini, mwakani tena michuano hii iwepo na ikiwezekana sasa iende kwenye mikoa mingine'', alisema.

Rais wa TBF Phares Magesa.

Michuano hiyo ambayo imefanyika kwa mara ya pili, imefikia tamati jana kwa mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars kushinda kwa 'Swipe' yaani mechi zote tatu kwenye'Best of 5' ya fainali dhidi ya Flying Dribbllers hivyo kutetea ubingwa wao.

Zawadi walizopata washindi jana ni milioni 3 kwa mshindi wa pili ambaye ni timu ya Flying Dribbllers, milioni 2 kwa Mchezaji bora wa mashindano 'MVP' Baraka Sadick na milioni 10 kwa mabingwa ambao ni Mchenga Bball Stars.