Wachezaji wa PSG wakishangili kufuzu hatua ya nusu fainali
PSG waliruhusu kufungwa bao 1-0 na Bayern Munich ya Ujerumani, goli lilifungwa na Eric Maxim Choupo Moting dakika ya 40 ya mchezo kwa kichwa kufuatia pasi ya David Alaba.
Ushindi huu haukuwafanya Bayern Munich kuweza kusonga mbele kutokana na faida ya goli la ugenini kufuatia mechi ya kwanza kumalizika kwa PSG kupata ushindi wa 3-2 nchini Ujerumani kwenye mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa na kufanya jumla kuwa 3-3.
PSG walipambana kujaribu kusawazisha hawakufanikiwa licha ya Kyllian Mbappe kufunga lakini mwamuzi akakataa goli kwa madai ya kuzidi,Neymar alikuwa katika kiwango bora sana pamoja na kukosa nafasi kadhaa za wazi za kufunga.
Chelsea wao walikubali kipigo dakika za mwisho kabisa za mchezo huku mashabiki wakiamini mechi inamalizika kwa suluhu, mshambuliaji Mehdi Taremi akafunga goli kwa staili ya kuvutia 'Acrobatic Kick' katika dakika ya 90+3.
Lakini matokeo ya mkondo wa kwanza ambayo Chelsea alishinda bao 2-0 ugenini yaliwapa faida kusonga mbele, hivyo basi wao watasubiri mshindi kati ya Liverpool na Real Madrid, huku PSG yeye akisubiri mshindi wa jumla kati ya Borussia Dortmund na Manchester City.
Chelsea kwa mara mwisho kutwaa ubingwa wa Ulaya ilikuwa msimu wa 2011/2012 walipowafunga Bayern Munich kwa mikwaju ya penalti. PSG hawajawahi kutwaa ubingwa lakini msimu uliopita walifanikiwa kucheza fainali na Bayern ambao wamewatoa sasa katika hatua ya robo fainali.