Alhamisi , 23rd Jun , 2016

Beki wa kushoto wa Yanga Oscar Joshua ameanza mazoezi mepesi katika kambi ya timu hiyo mjini Antalya, Uturuki kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe wiki ijayo.

Oscar aliumia kipindi cha kwanza cha mchezo dhidi ya Mo Bejaia na kushindwa kuendelea ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Mwinyi Hajji Mngwali ambaye naye akaonyeshwa kadi mbili mfululizo za njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90.

Yanga itawakaribisha Mazembe jumanne ijayo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huo ukiwa mchezo wa pili wa Kundi A baada ya jumapili kufungwa 1-0 na wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia jumapili.

Kambi ya Yanga imeingiwa na hofu ya kuingia kwenye mchezo na Mazembe bila beki halisi wa kushoto kutokana na Oscar kuwa majeruhi na wakati huo huo Mwinyi akiwa anatumikia adhabu ya kadi.

Kwa upande wa winga mpya wa Yanga Mzambia Obrey Chirwa naye ameanza mazoezi baada ya kuwasili akitokea Dar es Salaam alikorejea mara moja kushughulikia uhamisho wake.

Chirwa aliyesajiliwa wiki iliyopita kutoka FC Platinums ya Zimbabwe anatarajiwa kupewa nafasi katika mchezo dhidi ya Mazembe jumanne Dar es Salaam.

Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ambacho kinatarajiwa kurejea Ijumaa usiku ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.

Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Obrey Chirwa.Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.