Mwandembwa kuwa pilato Kariakoo Derby, Mei 8

Jumanne , 4th Mei , 2021

Bodi ya ligi imemtangaza Emmanuel Mwandembwa ndiye atakayekuwa mwamuzi wa kati katika mchezo wa ligi kuu wa Mei 8, 2021 wa watani wa jadi, Simba dhidi ya Yanga utakaochezwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa Jijino Dar es Salaam.

Mwamuzi wa kati, Emmanuel Mwandembwa aliyechaguliwa kuuchezesha mchezo wa watani wa jadi wa Simba dhidi ya Yanga.(wa pili kutoka kulia)

Mwandembwa atashirikiana na mwamuzi msaidizi namba moja, Frank Komba kutoka Dar es Salaam aliyetwaa tuzo ya mwamuzi msaidizi bora msimu uliopita, mwamuzi msaidizi namba mbili, Hamdani Saidi wa mkoani Mtwara.

Mwamuzi wa kati bora wa msimu uliopita wa VPL, Ramadhani Kayoko amechaguliwa kuwa mwamuzi wa akiba wa mchezo huo unatazamiwa kuwa wenye upinzani mkali kutokana na Utamaduni wa utaji wa jadi lakini pia kutokana na presha za kuwania ubingwa wa ligi kuu.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa Emmanuel Mwandembwa kuwa pilato wa mchezo huo mkubwa nchini na Afrika kiujumla, kwani msimu wa mwaka 2018 aliamua mchezo huo kwa kuonesha kuumudu vema.

Mwandembwa pia ana uzoefu wa kiasi wa kusimamia mchezo wa kimataifa kwani Agosti 11,  2019 alikuwa mwamuzi wa akiba kwenye mchezo wa klabu bingwa Afrika kati ya Aigle Noir ya Burundi dhidi ya wababe wa Kenya, Gor Mahia huku Elly Sasii wa Tanzania akiwa mwamuzi wa kati.