Jumanne , 6th Mei , 2014

Mwamuzi aliyechezesha pambano la Mgambo Shooting na ya Yanga ameondolewa katika orodha ya waamuzi wa ligi kuu kutokana na kitendo cha kumpekua mchezaji wa Mgambo kinyume na taratibu.

Mchezaji wa Mgambo Mohamed Neto

Bodi ya ligi ya soka Tanzania Bara TPLB imemwondoa Mwamuzi Alex Mahagi katika orodha ya waamuzi wa ligi kuu na Daraja la kwanza baada ya kubainika kukiuka maadili ya soka na uweledi wa waamuzi.

mwamuzi huyo ameondolewa kwa kosa la kumpekua mchezaji Mohamed Neto wa Mgambo Shooting katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara iliyomalizika mwezi uliopita kati ya timu ya Yanga na Mgambo Shooting mchezo uliopigwa katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Akiongea na Muhtasari wa michezo kuhusiana na Changamoto za ligi ya msimu wa 2013/14, Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Silas Mwakibinga amesema Mwamuzi huyo hakupaswa kumpekua mchezaji ndani ya uwanja hali iliyotafsiriwa ni kumdhalilisha mchezaji huyo.

Aidha Mwakibinga amesema baada ya mchezaji Neto kupekuliwa ilipelekea kugomea tukio hilo na hivyo mwamuzi kumtoa kwa kadi Nyekundu mchezaji huyo.