Jumapili , 28th Oct , 2018

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe ametangaza nauli ya basi kwenda kuishuhudia Taifa Stars itakapovaana na Lesotho wiki mbili zijazo.

Taifa Stars

Akizungumza katika kampeni maalum ya kuchangisha michango mbalimbali kwaajili ya kufanikisha safari hiyo, kampeni iliyofanyika jijini Dodoma, Waziri Mwakyembe amesema kuwa mpaka sasa jumla ya mabasi mawili yameshapatikana pamoja na nauli rasmi itakayotumika.

"Tumepata mabasi mawili kwenda Lesotho kwa nauli ya shilingi laki 1 na nusu,tunaendelea na mazungumzo na mashirika ya Ndege kupata nauli nafuu kwenda Lesotho", amesema.

"Kwa niaba ya TFF nimefarijika kwa msaada kutoka kwa serikali na mchango wa mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli", ameongeza.

Taifa Stars inatarajia kuweka kambi ya siku 10 nchini Afrika ya Kusini kabla ya kuelekea nchini Lesotho tayari kwaajili ya mchezo huo ambao utapigwa Novemba 18.

Shirikisho la soka nchini (TFF) kwa kushirikiana na serikali, inaendesha kampeni kwaajili ya kuiwezesha Taifa Stars ifuzu michuano ya mataifa ya Afrika nchini Cameroon mwaka 2019, ikiwa na kauli mbiu maalum ya #Afcon2019ZamuYetu.