
Jerry amefungiwa baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF mbele ya Kamati ya Ogunde.
Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.
Kwa kosa hilo akahukumiwa kuachana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja wakati shitaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
Katika shitaka hilo, Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na TP Mazembe Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya televisheni.
Jerry Muro amehukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao na inadaiwa hakutoa taarifa ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
Badala yake, imeelezwa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alifika mapema kabla ya kikao kwa ajili ya kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro hakuwepo ambapo Kamati ikaamua kuendelea na kikao kwa mujibu wa kanuni na hatimaye kuchukua hatua ilizochukua.
Hata hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF.