Jumanne , 23rd Oct , 2018

Mchezaji wa timu ya taifa ya kikapu ya wanawake nchini U18, Jescar Ngisaise amepata nafasi ya kufanya majaribio kwaajili ya kujiunga na kituo cha kukuza mchezo huo cha ligi ya kikapu ya Marekani NBA.

Jescar Ngisaise

Mchezaji huyo anatarajia kuondoka mapema Jumanne, Oktoba 23 kwenda nchini Senegal kwaajili ya majaribio hayo na endapo akifanya vizuri basi atapata nafasi ya moja kwa moja ya kujiunga na 'NBA academy'.

Kupata nafasi katika kituo hicho ni hatua moja kubwa kuelekea kucheza kwenye ligi ya kikapu ya wanawake ya Marekani 'WNBA'.

Jescar mwenye umri wa miaka 17 na nahodha wa timu ya taifa ya kikapu U18, amekua akifanya vizuri katika timu ya taifa na alichagulia katika timu ya All Stars kwenye mafunzo maalumu ya BWB yaliyofanyika Africa Kusini mwezi Agosti. 

Kwa upande wake, Jescar amesema, "Maandalizi yako vizuri, kwasasabu toka nianze kucheza kikapu najitahidi kama hivyo nilienda kwenye mashindano ya 'Basketball without border camp' na tena nimepata bahati hii ya kwenda Senegal kufanya majaribio, kama nikifuzu basi nitakuwa kule. Najiamini kwamba naweza ndio maana hizi nafasi zote zinatokea"

Hapa nyumbani, Jescar anacheza katika timu ya Ukonga Academy na katika ligi ya mkoa wa Dar es salaam iliyomalizika hivi karibuni na alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi hiyo.