Bondia Francis Miyeyusho 'chichi mawe'.
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania Mtanzania Francis Miyeyusho maarufu kama 'Chichi Mawe' mwishoni mwa juma lililopita alishindwa kuipeperusha vema bendera ya taifa baada ya kupoteza mpambano wake wa kimataifa wa raundi 12 kuwania ubingwa wa mabara wa UBO International akipambana na bondia toka nchini Czech.
Miyeyusho ambaye ni mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam alipoteza mpambano huo baada ya kupigwa kwa technical knock out (KO) na mpinzani wake Martin Parlagi katika mpambano uliopigwa mjini Plague Jamhuri ya Czech.
Kwa mujibu wa mratibu wa ndani wa mpambano huo katibu mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST) Antony Rutha amesema bondia huyo 'Chichi Mawe' alipoteza mpambano huo mapema katika raundi ya pili tu mara baada ya kupigwa ngumi ya tumbo na kujikuta akishindwa kuendelea na mpambano huo baada ya kuhisi maumivu makali ya tumbo na hivyo kumlazimisha mwamuzi kusimamisha mpambano huo na kumpa ushindi bondia Martin Parlag na kutwaa mkanda huo wa UBO kwa Mabara.
Kipigo hicho kinakuwa ni moja ya mwendelezo wa mabandia wengi wa ngumi za kulipwa nchini kushindwa kutamba katika mapambano wakiwa ugenini na kimsingi wadau wa ngumi wakiwemo mabondia wenyewe na viongozi wao na makocha wanatakiwa kujiuliza wapi wanajikwaa ama wanaangukia na kujikuta wakishindwa kufua dafu katika mchezo huo wakiwa ugenini.