Jumatano , 28th Mei , 2014

Mgombea Urais wa klabu ya Simba Michael Wambura amesema kuwa atakata rufaa kufuatia maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo kumuengua kwa madai kuwa si mwanachama halali wa klabu hiyo

Michael Richard Wambura.

Mgombea urais wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam bwana Michael Richard Wambura ambaye alienguliwa na kamati ya uchaguzi wa klabu hiyo kufuatia pingamizi liliyowekwa dhidi yake na baadhi ya wanachama wenzake, ameibuka leo na kusema atakata rufaa kwenye kamati ya rufaa za uchaguzi ya shirikisho la soka hapa nchini TFF.

Akiongea na waandishi wa habari klabuni, bwana Wambura amesema kimsingi kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo haikuwa sahihi kumuengua kwani waliomuwekea pingamizi hawakuwa wanachama halali wa klabu hiyo.

Bwana Wambura aliwataja wanachama wa tawi lililofutwa na uongozi wa Simba la Mpira pesa kwamba ndio walioweka mapingamizi ilhali wao sio wanachama halali wa klabu hiyo.

Hata hivyo, ilibidi Wambura afanye mkutano huo katika jengo la pili la klabu hiyo kufuatia jengo la kwanza ambalo hutumiwa kama ukumbi wa mikutano na ofisi za klabu hiyo kufungwa na baadhi ya wanachama wakimshutumu katibu mkuu wao bwana Ezekiel Kamwaga kwamba ana njama ya kutorosha baadhi ya nyaraka muhimu za klabu hiyo.