Jumatatu , 11th Dec , 2017

Shirikisho la soka barani Ulaya leo limefanya droo ya kupanga mechi za hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA ambapo Mabingwa watetezi Real Madrid wataanzia Bernabeu kuikaribisha Paris Saint-Germain PSG.

Katika droo hiyo pia mabingwa wa England Chelsea, wataanzia nyumbani kuwakaribisha vinara wa La Liga FC Barcelona. Kikubwa katika mchezo huu ni mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi akiwa hajawahi kuifunga Chelsea katika mechi nane alizokutana na timu hiyo na kufanya Chelsea iwe ndio timu ambayo amecheza nayo mara nyingi zaidi bila kuifunga.

Vinara wa EPL Mamchester City itaanzia ugenini dhidi ya FC Basel. Manchester United itakuwa ugenini kucheza na Sevilla ya Hispania. Mchezo mwingine utawahusisha wanafainali wa msimu uliopita Juventus ya Italia ambayo itaanzia nyumbani dhidi ya Tottenham.

Mabingwa mara tano wa UEFA Liverpool itasafiri hadi Ureno kucheza na FC Porto. Bayern Munich itaanzia nyumbani kwenye dimba la Allienz Arena kucheza na Besiktas ya Uturuki. Shaktar Donetsk ya Uturuki itakuwa nyumbani kuanza na AS Roma.

Neymar Jr anarejea kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Hispania kikazi akiwa na PSG kuikabili Real Madrid. Msimu uliopita PSG iliondolewa na Barcelona kwa kufungwa jumla ya mabao 6-5 wakati huo Neymar akiwa na Barcelona.