Jumatatu , 18th Sep , 2023

Uongozi wa Yanga SC utatoa heshima kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa dakika 1, ikiwa ni kuwashuru kwa kuiunga mkono timu yao kwa kusafiri kwa idadi kubwa kwenda nchini Rwanda.

Afisa habari wa klabu hiyo Ally Kamwe amethibitisha kuwa watatoa heshima hiyo dakika ya 12 ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo.

 

"Dakika ya 12 ya mchezo wetu wa Jumatano dhidi ya Namungo FC, tutasimama kwa Dakika 1 kuwashukuru Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa Klabu yetu waliosafiri kwenda Kigali, Rwanda na kutengeneza historia hii kubwa ya kuwa na Mashabiki wengi kwenye mchezo wa Ugenini. Na Viongozi wetu wamewaandalia Surprise kubwa Mashabiki wetu dakika hiyo ya 12 ya mchezo wetu dhidi ya Namungo na hii siyo ya kukosa" Amesema Ally Kamwe 

Zaidi ya magari 40 aina ya Costa ya mashabiki wa Yanga yalisafiri kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya kuiunga mkono timu yao na kuongeza hamasa. Yanga  ilicheza nchini Rwanda mchezo wa mkondo wa kwanza wa klabu bingwa Afrika dhidi ya EL Merrikh mchezo ambao ilishinda  kwa mabao 2-0.

 

Kikosi hicho kitashuka tena Dimbani Jumatano Septemba 20 kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC, mchezo huu utachezwa Saa 1:00 Usiku, uwanja wa Azam Complex.