Manuel Neuer aweka historia ya kibabe Ujerumani

Jumanne , 8th Jun , 2021

Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Ujerumani, Manuel Neuer ameweka rekodi ya kuwa kipa pekee katika historia ya timu hiyo kufikisha michezo 100 baada ya usiku wa jana kuchezamchezo wa kirafiki dhidi ya Latvia ambapo Ujerumani iliibuka na ushindi mnono wa mabao 7-1.

Mlinda mlango wa Ujerumani, Manuel Neuer akipigiwa makofi ya heshima na wachezaji wenzake kabla ya mchezo wa usiku wa jana dhidi ya Latvia kwa kufikisha michezo 100 akiwa kipa pekee kufanya hivyo katika timu hiyo.

Kabla ya mchezo huo kuanza, Shirikisho la soka la nchini Ujerumani 'DFB', lilimuandalia medali ya dhahabu ya heshima mlinda mlango huyo bora duniani kwa mafanikio hayo makubwa ya kihistoria yaliyopambwa na kubeba kombe la Dunia la mwaka 2014 nchini Brazil.

Neuer mwenye miaka 35, pia alivaa glavu maalum zilizoandikwa '100' zikimaanisha michezo 100 ambayo ameichezea timu hiyo kwenye mchezo huo ambao hautakaa usahaulike kwenye maisha yake ya ska kutokana na kupokea pongezi nyingi za kuthamini mchango wake mkubwa.

(Manuel Neuer akiwa amevaa glavu maalum zilizoandikwa '100' kumaanisha idadi ya michezo ya kihistoria aliyoiweka kwenye taifa hilo baada ya mchezo wa usiku wa jana dhidi ya Latvia)

Neuer alianza kuichezea timu ya taifa ya Ujerumani tarehe 2 Juni 2009 kwenye mchezo dhidi ya Falme ya Kiarabu ya Emirates kwenye uwanja wa Al-Maktoum, Dubai akiwa kipa wa klabu ya Schalke 04 kabla ya kuhamia klabu yake ya sasa ya Bayern Munich.

Baada ya mchezo kumalizika, Neuer amesema “Ninafuraha sana na wachezaji wenzangu na sina mpango wa kustaafu soka”, kauli ambayo inadhihirisha nyota huyo bado yupo yupo sana kwenye timu hiyo.

Kwenye mchezo huo, mabao ya Ujerumani yalifungwa na Robin Gosens dk19', Ilkay Gundogan dk20', Thomas Mueller dk27', Robert Ozols aliyejifunga dk36', Serge Gnabry dk45', Timo Werner dk50', Latvia walipata moja la kufutia machozi Aleksejs Saveljevs dk75 na la saba likifungwa na Leroy Sane dk76.

Ujerumani imecheza mcehzo huo kujiweka sawa na michuano ya UEFA EUROS 2020 inayotaraji kuanza 11 Juni 2021 huku ikiwa kundi moja na Mabingwa watetezi wa Dunia, Ufaransa, bingwa mtetezi wa michuano hiyo timu ya taifa ya Ufaransa, Ureno na Hungary.