
Aliyekuwa kiungo wa Simba, Francis Kahata akishangilia moja ya bao alilofunga kwenye VPL msimu uliopita.
Kahata ameyasema hayo usiku wa jana Juni 4, 2021 kupitia kipindi cha michezo cha East Africa Redio, 'KIPENGA' na kusema hakuna aijuae kesho huenda akasalia nchini kukipiga.
“Kuondoka kwangu Simba haina maana ndiyo mwisho wangu kuishi Tanzania. Huwezi kujua leo au kesho unaweza kusikia nipo katika klabu nyingine”. Kahata amesema.
Kiu ya wafuatiliaji wa soka nchini ni kutaka kujua mkali huyo wa kupiga pasi atatimkia kwenye klabu gani kati ya Yanga ama Azam ambayo inahusishwa naye kikaribu.
Katika kujibia hilo Kahata amesema; “Kuhusu Azam naomba usinilishe maneno” akiwa na maana ya kwamba hana maana kwamba amesema au amejiunga na klabu ya Azam.
Kahata amekiri kuwa, majeraha aliyoyapata na kumlazimu kukaa nje kwa muda mrefu yamefanya apoteze nafasi kwenye kikosi hicho cha kwanza na hata aliporejea alikuta upinzani mkali muda ambao hakuwa timamu kimwili.
Mwisho akamaliza kwa kuwashukuru wanasimba na wote waliokuwa wana muunga mkono wakati alipokuwa anaitumikia Simba misimu miwili iliyopita tokea asaini kandarasi ya maika miwili kuanzia mwaka 2019 akitokea klabu ya Gor Mahia ya Kenya.