Jumatatu , 24th Mei , 2021

Taarifa kutoka Hispania zinaripoti kuwa mshambuliaji wa Real Madrid Eden Hazard anataka kuondoka klabu hapo kwenye dirisha kubwa la usajili linalofata na inatajwa kuwa hana furaha na huenda akarejea katika timu yake ya zamani Chelsea ya England.

Eden Hazard

Ukiachana na kutokuwa na furaha lakini pia inaripotiwa kuwa mshambuliaji huyo raia wa Ubeligi anahofia nafasi yake ndani ya kikosi hicho endapo kama Real Madrid itakamilisha usajili wa Kylia Mbappe kutoka PSG kwenye dirisha la usajili linalofata.

Hazard alijiunga na Real Madrid Juni, 2019 akitokea Chelsea kwa ada ya uhamisho ya fedha za Uingereza Pauni million 100 ambayo ni zaidi ya Bilioni 327 kwa pesa za kitanzania na alisaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo mpaka mwaka 2024.

Lakini mchezaji huyo hajafanikiwa kukifanya kile ambacho kilitegemewa na wengi, amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara na tangu ajiunge na Madrid amecheza jumla ya michezo 43 na amefunga mabao matano (5) tu huku akitoa pasi za usaidizi wa mabao nane (8) ndani ya misimu miwili.

Inaaminika kuwa Real Madrid wameanza kupoteza imani na mchezaji huyo kutokana na kutopatikana muda mwingi wa msimu kutokana na majeruhi kwenye misimu yote miwili na hivi sasa pia amepata maumivu tena ambayo yalimfanya akosekane kwenye mchezo wa mwisho wa ligi ambao ulikuwa muhimu kwenye kuwania ubingwa dhidi ya Villarreal.

Na klabu ya Chelsea ndio itakuwa kipaumbele kwa Eden Hazard endapo kama atafikia uamuzi wa kuondaka Santiago Bernabeu.