Jumatatu , 18th Jun , 2018

Timu ya taifa ya Ubeligji imeibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Panama kwenye mchezo wa Kundi G kwenye Fainali za Kombe la Dunia ambao umemalizika usiku huu.

Mabao mawili yaliyofungwa na mshambuliaji wa Manchester United Romelu Lukaku na bao moja la winga wa klabu ya Napoli Dries Mertens, yametosha kuifanya Ubeligji kuwa timu ya pili kushinda kwa mabao mengi baada ya Urusi.

Kwa upande mwingine nyota wa Manchester City na mfalme wa 'Assist' kwenye EPL msimu uliopita Kevin De Bruyne amesaidia bao la Lukaku na la pili kwa Ubeligji huku Eden Hazard akisaidia bao la tatu kwa Ubeligji na la pili kwa Lukaku.

Naye winga Dries Mertens amekuwa Mbeligji wa kwanza kufunga kwenye fainali mbili tofauti za Kombe la Dunia (2014 na 2018), tangu afanye hivyo nyota mwingine Steller Wilmots aliyefunga mwaka 1998 na 2002.

Pia Ubeligji imefikisha mechi 20 bila kufungwa ambapo imeshinda mechi 15 na kutoka sare 5. Sasa inaongoza Kundi G lenye timu za England, Panama na Tunisia.